Maana ya Ijumaa Kuu kwa Wakristo: Ibada, Tafakari na Kutokula Nyama Kama Ishara ya Heshima | Maadhimisho ya Ijumaa Kuu: Wakristo wanamkumbuka Yesu Kristo kupitia ibada, kutafakari, na kujitolea.
Wakristo duniani kote wanaadhimisha Ijumaa Kuu ikiwa ni siku maalum ya kumkumbuka Bwana Yesu Kristo kwa mateso na kifo chake msalabani. Ni siku ya umuhimu wa kiroho, ambayo waumini hukusanyika makanisani kwa ibada maalum, sala za toba, tafakari ya kibinafsi na kujizuia kula au kunywa, haswa nyama nyekundu, kama ishara ya heshima na maombolezo.
Katika Kanisa Katoliki na madhehebu mengine ya Kikristo, waumini hujiepusha kula aina yoyote ya nyama, ikiwa ni pamoja na nyama ya ng’ombe, mbuzi, au sungura. Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Method Kilaini alisema Ijumaa Kuu ni siku ya maombolezo ya mateso ya Kristo, na hivyo kutokula nyama ni njia ya kumkumbuka aliyemwaga damu yake kwa ajili ya wokovu wa binadamu.
Maana ya Ijumaa Kuu kwa Wakristo: Ibada, Tafakari na Kutokula Nyama Kama Ishara ya Heshima
Kwa mujibu wa mafundisho ya Kanisa, Ijumaa Kuu huadhimishwa Ijumaa kabla ya Pasaka ambayo mwaka huu inaadhimishwa Jumapili ya Aprili 20. Kwa mujibu wa Injili, Yesu Kristo alisulubishwa siku ya Ijumaa na kufufuka tena siku ya tatu ambayo ndiyo msingi wa imani ya Kikristo.
Katibu mtendaji wa Idara ya Liturujia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Dk Clement Kihiyo alieleza kuwa tabia ya kutokula nyama siku ya Ijumaa Kuu inatokana na mila za Kiyahudi, ambapo mtu anapokufa kwa kumwaga damu, jamii huacha kula nyama kwa heshima ya marehemu.
Aidha Padre Kihiyo alisema nyama ni chakula cha anasa na cha gharama, hivyo kujiepusha na nyama kunasaidia waumini kuwa wanyenyekevu na kuwasaidia wenye uhitaji. Ijumaa kuu pia hutumika kwa maombi maalum yanayohusu nyanja zote za maisha na kutoa heshima kwa msalaba, ishara ya wokovu kwa Wakristo.
Kwa upande wake Padre Pascha Ighondo wa Vatican ameeleza kwamba, msalaba wa Yesu Kristo si tu chombo cha mateso, bali ni kielelezo cha huruma, upendo, neema, msamaha na matumaini ya uzima wa milele. Aliwahimiza waamini kumtafakari Kristo, aliyejitoa kwa ajili yao, na kuishi maisha ya utakatifu.

Padre Revocatus Paul wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Mtume Dar es Salaam naye alisisitiza kuwa Ijumaa kuu ni siku ya amani, tafakari na ibada na si siku ya kuadhimisha. Alieleza kuwa ulaji wa nyama unatafsiriwa kuwa ni ishara ya kusherehekea jambo ambalo haliendani na roho ya siku hizo.
Katika kuadhimisha Ijumaa Kuu mwaka huu, Baba Mtakatifu Francisko ametembelea Gereza la Regina Caeli lililopo Roma, ikiwa ni desturi ya kuwaosha wafungwa miguu kwa kufuata mfano wa Yesu Kristo aliyewaosha miguu wafuasi wake kabla ya mateso yake.
Monsinyo Kilaini amewataka waamini wote kuonesha matumaini, mshikamano na upendo hasa ikizingatiwa kuwa, Kanisa Katoliki limeutangaza mwaka 2025 kuwa ni Mwaka Mtakatifu wenye kauli mbiu “Mahujaji wa Matumaini”. Aliwataka Wakristo kujiandaa na sikukuu ya Pasaka kwa kuishi maisha ya haki na upendo ili kujenga dunia yenye amani.
CHECK ALSO:
Weka maoni yako