Gharama za Kujiandikisha Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) | Gharama ya Kujandikisha kama Private Candidate Mtihani wa Form Four NECTA
Gharama za Kujiandikisha Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE)
Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetoa maelezo kuhusu gharama na hatua za usajili kwa wanafunzi wa kujitegemea wanaotarajia kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) mwaka 2024. Kujua gharama na muda wa kujiandikisha ni muhimu ili kujiandaa kwa mtihani kwa ufanisi na kuepuka gharama za kuchelewa.
1. Gharama za Kawaida za Usajili wa CSEE 2024
Kwa mujibu wa NECTA, usajili wa kawaida utaanza tarehe 1 Januari 2024 na kumalizika tarehe 29 Februari 2024. Gharama ya usajili kwa watahiniwa wa kujitegemea itakuwa Shilingi 50,000 kwa wanaojiandikisha kwa ajili ya Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE). Kwa upande wa Upimaji wa Kidato cha Pili (FTNA), ada itakuwa Shilingi 10,000.
2. Gharama za Usajili wa Kucherewa
Kwa wale watakaokosa kipindi cha usajili wa kawaida, NECTA imeweka kipindi maalum cha usajili wa kuchelewa ambacho kitaanza tarehe 1 Machi 2024 hadi 31 Machi 2024. Watahiniwa watakaosajili katika kipindi hiki watalazimika kulipa ada ya ziada, ambapo ada ya Mtihani wa Kidato cha Nne itakuwa Shilingi 65,000, wakati ada ya FTNA itakuwa Shilingi 15,000.
3. Vigezo vya Mtahiniwa Kujisajili kwa CSEE
Ili kujisajili kwa mtihani wa CSEE kama mtahiniwa wa kujitegemea, ni lazima mhusika awe na sifa zifuatazo:
- Kurudia mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE), au
- Kufaulu Mtihani wa Maarifa (QT) katika kipindi kisichozidi miaka kumi iliyopita, au
- Kufaulu Upimaji wa Kidato cha Pili (FTNA) katika kipindi kisichozidi miaka kumi iliyopita, au
- Kuwa na sifa zinazolingana na hizo kutoka nje ya nchi, zilizothibitishwa na Baraza la Mitihani la Tanzania.
Kwa watakaotaka kufanya Upimaji wa Kidato cha Pili (FTNA), wanatakiwa kuwa wanatafuta sifa ya kujiandikisha kama watahiniwa wa kujitegemea wa CSEE.
4. Utaratibu wa Usajili wa Mtihani wa CSEE 2024
NECTA imeweka mwongozo wa hatua za kufuata kwa watahiniwa wa kujitegemea katika usajili wa mtihani:
- Hatua ya Kwanza: Tembelea kituo cha mtihani unachotarajia kufanya mtihani wako ili kupata maelekezo muhimu kutoka kwa Mkuu wa Kituo.
- Hatua ya Pili: Mkuu wa Kituo cha Watahiniwa wa Kujitegemea ataingiza namba yako kwenye mfumo wa usajili wa mtandaoni ili kupata ‘Control Number’ kwa ajili ya kufanya malipo ya ada.
- Hatua ya Tatu: Fanya malipo ya ada kwa kutumia Control Number uliyopewa. Malipo yanaweza kufanyika kupitia benki za NMB, CRDB, au NBC.
- Hatua ya Nne: Baada ya malipo, rudi kwa Mkuu wa Kituo ili kukamilisha usajili wa mtihani. Hakikisha una vielelezo vyote vinavyohitajika kama vile picha, cheti cha kuzaliwa, orodha ya masomo ya kusajiliwa, na namba ya simu.
- Hatua ya Tano: Baada ya usajili kukamilika, utapewa nakala ya fomu yako kwa ajili ya kumbukumbu. Nakala zingine zitabaki katika kituo na Baraza la Mitihani.
5. Umuhimu wa Kujisajili Mapema
NECTA imehimiza watahiniwa kujisajili mapema ili kuepuka usumbufu wa kujiandikisha dakika za mwisho na kuepuka ada ya kuchelewa. Mfumo wa usajili unapatikana katika tovuti rasmi ya NECTA, www.necta.go.tz, ambapo maelekezo zaidi kuhusu usajili yanapatikana.
Mapendekezo ya Mhariri:
Weka maoni yako