Orodha Kamili ya Masomo ya Mitihani ya NECTA Kidato cha Nne
Mitihani ya Kidato cha Nne, inayojulikana kama CSEE (Certificate of Secondary Education Examination), ni mojawapo ya mitihani muhimu zaidi kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini Tanzania. Mitihani hii hufanyika kila mwaka katika wiki ya kwanza ya mwezi Novemba na inawalenga wanafunzi waliomaliza miaka minne ya elimu ya sekondari. Katika makala hii, tutajadili kwa undani orodha ya masomo yanayofanyiwa mtihani, pamoja na umuhimu na malengo ya mitihani hii ya kitaifa.
Malengo ya Mitihani ya Kidato cha Nne (CSEE)
Mitihani ya CSEE imeundwa kwa madhumuni makuu yafuatayo:
- Kupima Ujuzi na Maarifa: Mitihani hii hutathmini ujuzi na maarifa ambayo mwanafunzi ameyapata katika masomo mbalimbali wakati wa masomo yake ya sekondari. Hii inajumuisha uwezo wa mwanafunzi kutumia maarifa hayo kutatua changamoto za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiteknolojia kwa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla.
- Kutambua Wanafunzi Wenye Uwezo wa Kuendelea na Elimu ya Juu: Matokeo ya mitihani hii husaidia kuchagua wanafunzi wenye sifa za kuendelea na masomo ya kidato cha tano au vyuo vya elimu ya juu.
- Kuchangia Maendeleo ya Taifa: Mitihani hii inalenga kumjenga mwanafunzi kuwa na uwezo wa kuchambua, kutumia, kutathmini, na kuchangia maendeleo katika nyanja mbalimbali za maisha.
Sifa za Wanafunzi Wanaofanya Mitihani ya Kidato cha Nne
Ili mwanafunzi aweze kufanya mtihani wa CSEE, ni lazima awe ametimiza masharti yafuatayo:
- Amemaliza miaka minne ya masomo ya sekondari katika shule iliyosajiliwa, iwe ya serikali au ya binafsi.
- Amepita mtihani wa Kidato cha Pili au amefaulu mtihani wa Qualifying Test (QT).
- Wanafunzi wanaorudia mtihani wa Kidato cha Nne wanaweza kujisajili kama watahiniwa binafsi.
Orodha ya Masomo ya Mitihani ya NECTA Kidato cha Nne
Watahiniwa wa CSEE husajiliwa katika masomo mbalimbali kulingana na mchepuo waliouchagua wakiwa kidato cha tatu. Kuna masomo ya msingi ambayo ni ya lazima kwa kila mwanafunzi, na pia kuna masomo ya ziada yanayochaguliwa kulingana na mchepuo wa mwanafunzi.
Masomo ya Lazima
Masomo ya lazima kwa watahiniwa wote wa CSEE ni:
- Civics (Uraia)
- History (Historia)
- Geography (Jiografia)
- Kiswahili
- English Language (Lugha ya Kiingereza)
- Biology (Bailojia)
- Basic Mathematics (Hisabati ya Msingi)
Masomo ya Ziada
Mbali na masomo ya lazima, wanafunzi wana fursa ya kuchagua masomo ya ziada ili kukamilisha sifa za mchepuo wao. Masomo haya yanajumuisha sayansi asilia, biashara, uchumi wa nyumbani, na ufundi.
- Masomo ya Sayansi: Fizikia, Kemia.
- Masomo ya Biashara: Uhasibu (Book Keeping), Biashara (Commerce).
- Masomo ya Uchumi wa Nyumbani: Chakula na Lishe (Food and Nutrition), Ususi na Ushonaji (Textile and Dress Making).
- Masomo ya Ufundi: Ujenzi (Building Construction), Uchoraji wa Majengo (Architectural Draughting), Useremala (Carpentry and Joinery), Ufundi wa Mabomba (Plumbing), Ufundi wa Umeme (Electrical Installation), Ufundi Mitambo (Workshop Technology), na mengine mengi.
- Elimu ya Dini: Elimu ya Dini ya Kikristo (Bible Knowledge), Elimu ya Dini ya Kiislamu.
- Sanaa: Sanaa ya Ufundi (Fine Art), Muziki, Sanaa za Maonyesho.
- Lugha za Kigeni: Kifaransa (French), Kiarabu (Arabic), Fasihi ya Kiingereza (Literature in English).
- Masomo Mengine: Kilimo, Sayansi ya Kompyuta (Information and Computer Studies), Hisabati ya Ziada (Additional Mathematics).
Mwongozo wa Uchaguzi wa Masomo
Mwanafunzi anatakiwa kuchagua masomo kulingana na mchepuo aliochagua shuleni, na ni muhimu kuhakikisha kuwa haorodheshi zaidi ya masomo kumi kwa mtihani wa CSEE. Wanafunzi wanashauriwa kuchagua masomo yanayofanana na malengo yao ya baadaye kielimu au kitaaluma. Kwa mfano, mwanafunzi mwenye ndoto za kujiunga na masomo ya sayansi ya afya au anaetaka kuwa mhandisi kwa ngazi za elimu ya juu, anapaswa kujisajili katika Masomo ya Sayansi kama vile Fizikia, Kemia.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Orodha ya Masomo Shule ya Msingi
- Jinsi ya Kujiandaa na Mtihani wa NECTA- Mwongozo Kamili
- TCU Yatangaza Dirisha la Tatu la Udahili Vyuo Vikuu 2024/2025
- Sifa Za Kujiunga Na Mafunzo Ya Ualimu
- Alama za Ufaulu Kidato cha Sita: Viwango na Maelezo Muhimu
- Sifa za Watahiniwa wa Kujitegemea Kidato cha Sita
- Sifa za Watahiniwa wa Kujitegemea Kidato cha Nne
Weka maoni yako