Umuhimu wa Masomo ya Pre-form One

Umuhimu wa Masomo ya Pre-form One

Masomo ya kujiandaa na elimu ya kidato cha kwanza, almaarufu kama Pre-Form One, ni moja kati ya masomo yaliyojizolea umaarufu mkubwa nchini Tanzania. Wazazi wengi huamua kuwaandikisha watoto wao waliohitimu elimu ya shule ya msingi kwa lengo la kuwaandaa na ngazi mpya ya elimu ya sekondari. Kozi hii ya awali imejikita katika kuwasaidia wanafunzi kuwa na msingi mzuri katika masomo mbalimbali na kujiandaa na mazingira ya sekondari ambayo yanatofautiana sana na shule za msingi.

Umuhimu wa Masomo ya Pre-form One

Kwa Nini Masomo ya Pre-Form One Ni Muhimu?

Masomo ya Pre-Form One yanatolewa nyingi hutolewa mara tu baada ya wanafunzi wa darasa la saba kufanya mitihani yao ya kumaliza elimu ya shule ya Msingi, hivyo yanakuwa ni daraja la kuunganisha elimu ya msingi na sekondari.

Kozi hii inafundisha masomo kama Hisabati, Jiografia, Kiswahili, Kiingereza, Uraia na Sayansi. Hii husaidia wanafunzi kuwa na ufahamu wa awali wa masomo haya katika kiwango cha sekondari, na kuwafanya kuanza kidato cha kwanza wakiwa na ujasiri zaidi.

Maandalizi ya Kisaikolojia na Kijamii

Masomo ya Pre-Form One huwasaidia wanafunzi kujenga nidhamu na kuwa na ratiba rasmi ya masomo kabla ya kuanza sekondari. Hili linawasaidia kuwa tayari kisaikolojia na kuwapa nafasi ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wanapoanza masomo rasmi ya kidato cha kwanza. Kwa baadhi ya wanafunzi, muda wa miezi minne wa kusubiri kuanza sekondari unaweza kuwa na changamoto nyingi iwapo wataachwa nyumbani. Kozi hii huwasaidia kuepuka mivuto mibaya na badala yake kuwapa majukumu muhimu ya kielimu.

Faida kwa Wanafunzi: Kujiandaa na Lugha na Mtaala wa Sekondari

Wanafunzi wengi wa shule za msingi hufundishwa kwa lugha ya Kiswahili. Kwa kuwa sekondari hutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia, masomo ya Pre-Form One huwa fursa muhimu kwao kuboresha lugha hiyo.

Hii huwasaidia kuepuka changamoto za lugha wanapoanza sekondari, na kuwapa msingi mzuri wa kuelewa masomo kama Sayansi na Hisabati, ambayo hufundishwa kwa Kiingereza. Wanafunzi kama Kulawa Raymond wamesisitiza umuhimu wa kozi hii katika kuwasaidia kuboresha uelewa wao wa Kiingereza, ambayo ni muhimu kwa maendeleo yao ya kielimu.

Wazazi na Gharama za Kozi za Pre-Form One

Ingawa kozi hizi zina umuhimu mkubwa, gharama zake zimekuwa zikionekana kama changamoto kwa baadhi ya wazazi. Uchunguzi unaonyesha kuwa wanafunzi hulipa kati ya shilingi 20,000 hadi 100,000 kwa mwezi kwa masomo ya Pre-Form One, na shule nyingine hutoza karo kwa mkupuo kwa kipindi cha miezi mitatu au minne. Kwa mfano, shule ya sekondari Mukombozi katika mkoa wa Kagera hutoa kozi hii bure huku ikilenga wanafunzi wenye nia ya kusoma masomo ya sayansi. Hata hivyo, baadhi ya shule na vituo vya masomo vinatoza ada za usajili na gharama za chakula ili kuwasaidia wanafunzi kuwa na mazingira bora ya kujifunza.

Changamoto za Kozi za Pre-Form One

Pamoja na umuhimu wa masomo haya, baadhi ya vituo vya masomo hayana sifa za kutosha kutoa elimu yenye kiwango kinachostahili. Baadhi ya vituo vinavyotoa kozi za Pre-Form One vinadaiwa kutumia walimu ambao hawajahitimu ipasavyo na hawana ujuzi wa kutosha, na hivyo kuwanyima wanafunzi fursa ya kupata elimu bora.

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Hamis Lissu, alieleza kuwa kozi hizi hazifuatiliwi na serikali bali hutolewa kwa makubaliano ya wazazi na shule au vituo husika. Hii inaleta changamoto kwa wazazi katika kuchagua kituo bora kwa ajili ya watoto wao.

Mtazamo wa Wataalamu wa Elimu

Baadhi ya wataalamu wa elimu wanaona kozi hizi kuwa ni sehemu ya “fasheni” kwa wazazi, huku wakihoji faida halisi ya masomo haya kwa watoto. Kwa mfano, Dk. Joviter Katabalo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anahisi kuwa badala ya muda mwingi kutumika kwenye masomo ya Pre-Form One, watoto wangepaswa kufundishwa stadi za maisha kama vile kazi za nyumbani na kujitegemea, jambo ambalo lingewasaidia zaidi kwa maisha ya baadaye. Hata hivyo, wazazi wengi wanaona kuwa masomo haya ni njia bora ya kuwaweka watoto wao katika njia sahihi ya masomo ya sekondari.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Vitu Muhimu vya Kuzingatia Wakati wa Kuchagua Shule
  2. Ubunifu ulivyo Changia Ufaulu wa Wanafunzi Darasa la Saba
  3. Alama za Ufaulu Shule za Msingi (Darasa la Saba) Tanzania
  4. NECTA Yatangaza Matokeo ya Mtihani wa Darasa la Saba (Psle) 2024
  5. Orodha ya Masomo ya Darasa La Saba