Yanga Kutambulisha Jezi Mpya za Msimu 2025/26 Leo | Yanga imepanga kutambulisha jezi zake mpya za msimu ujao siku ya leo, Jumapili, Agosti 24, 2025.
Yanga Kutambulisha Jezi Mpya za Msimu 2025/26 Leo
Utambulisho huo wa jezi mpya za Yanga utafanyika siku tatu kabla ya uzinduzi wa jezi za watani wao wa jadi, Simba ambao utafanyika Agosti 27, 2025.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema kuwa uzinduzi wa jezi hizo utaenda sambamba na uuzaji wake.
“Siku ya leo (Jumapili) klabu yetu ya Yanga inakwenda kuzindua jezi zake za msimu wa 2025/2026. Muda ambao klabu yetu inakwenda kuzindua jezi ni saa 6:00 mchana.
“Baada ya kuzindua tutaanza kuuza. Tutazizindua hizi jezi kwa njia ya kimtandao. Tukishazindua jezi, kauli mbiu yetu inasema tunazindua, tunauza,” amesema Kamwe.
Uzinduzi wa jezi hizo ni sehemu ya maandalizi ya Yanga kwa ajili ya msimu mpya wa 2025/2026 ambao itakuwa na kibarua cha kutetea mataji matatu makubwa ambayo ilichukua msimu uliopita.

Mataji hayo ni Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho la CRDB na taji la Ngao ya Jamii.
Taji la Ngao ya Jamii, Yanga italitetea kwa kukabiliana na Simba katika mchezo uliopangwa kufanyika Septemba 16, 2025 kwa mujibu wa kalenda ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).
Yanga pia inakabiliwa na mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ambayo msimu uliopita iliishia hatua ya makundi.
Katika msimu wa 2025/2026, Yanga imepangwa kuanzia raundi ya kwanza ya awali ambapo itakabiliana na Wiliete Benguela ya Angola.
Kama Yanga ikifanikiwa kusonga mbele, katika raundi ya pili itakabiliana na mshindi baina ya Silver Strikers ya Malawi au Elgeco Plus ya Madagascar.
SOMA PIA:
Weka maoni yako